Muongozo huu ambao unapatikana kwa lugha zote mbili za Kiingereza na Kiswahili umepangwa kutoa mwongozo kwa wanajamii na watumizi wa rasilimali ambao wangependa kusimamia rasilimali zao kwa kuanzisha mikakati ya usimamizi wa kijamii wa maeneo ya mwambao na rasilimali za baharini. Haijadhamiriwa uwe muongozo unaokwenda hatua kwa hatua lakini ni kama utangulizi wa mifano muhimu na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika uanzishwaji wa usimamizi wa kijamii. Muongozo unatoa mwanga wa maeneo mengine kwa wale ambao wangependa kupata maelekezo zaidi au kuomba msaada na kuona mifano ya kivitendo.
Chapisho hili limetolewa na Mradi wa Kuimarisha maeneo ya Hifadhi ya Afrika Mashariki unaotekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanasayansi wa Ukanda wa Magharibi ya Bahari ya Hindi (WIOMSA), Chuo Kikuu cha Rhode Island (URI) na Blue Ventures (BV), Shirika la Wanyamapori, Kenya (KWS) na Kitengo cha Hifadhi ya Bahari and Maeneo tengefu (MPRU). Msaada wa fedha umetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje (State Department) ya Serikali ya Marekani.